Trending Now

VIJANA WAHIMIZWA KUTOKUBALI KUTUMIKA KUVUNJA AMANI.

 

VIJANA WAHIMIZWA KUTOKUBALI KUTUMIKA KUVUNJA AMANI


Na Mwandishi Wetu.

Vijana nchini wamehimizwa kuepuka kutumika na baadhi ya watu wasio na nia njema ili kuvunja Amani ya Nchi hatua itakayosababisha maendeleo ya Taifa kuzorota.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoshughulikia masuala ya Demokrasia ya Vyama vingi nchini katika Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini na Wadau wa Demokrasia Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na hali ya Siasa Nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam.

Dkt. Yonazi amesema vijana wana sehemu kubwa ya kuwajibika kuhakikisha Taifa husika linapata maendeleo na siyo kutumika kwa lengo la kuvunja mshikamano, umoja na upendo ulioanzishwa na waasisi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoshughulikia masuala ya Demokrasia ya Vyama vingi katika Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam.

“Kuhusu ushiriki wa vijana katika Siasa, Demokrasia na Uongozi Kikosi Kazi kilipendekeza kuwa, juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa, demokrasia, uongozi, uchumi, ulinzi na usalama wa nchi yetu ziendelee na mikakati mipya ibuniwe ili kuongeza ufanisi na tija,” amesema Dkt. Yonazi.

Pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha Mikakati iliyopo na mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana pamoja na mipango ya kuhamasisha ushiriki wa vijana katika siasa, demokrasia, uongozi, uchumi, ulinzi na usalama wa nchi.

Kuhusu elimu ya uraia Katibu MKuu huyo amebainisha kwamba ipo haja ya elimu ya uraia kutolewa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa na kuwa na uelewa wa pamoja wa walengwa na elimu ya mpiga kura ifundishwe katika ngazi zote za mfumo wa elimu kuanzia shule za awali mpaka katika vyuo vya elimu ya juu.

“Serikali na wadau wengine waongeze kiwango cha ufadhili katika kutoa elimu ya uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura, ili kukabiliana na upungufu wa rasilimali fedha, watu na vifaa katika kutoa elimu hiyo,” Amebainisha Katibu Mkuu huyo.

Aidha amehimiza ushirikishwaji wa Watu Wenye Ulemavu katika Siasa, Demokrasia na Uongozi kwa kuzifanyia maboresho Sheria zisizozingatia ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu akisema huzuia ushiriki wao katika siasa, demokrasia na uongozi ndani ya vyama siasa.

Baadhi ya Wenyeviti wa Vyama vya Siasa nchini wakifuatilia mjadala wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika  Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Wakuu wa Taasisi wakifuatilia mjadala wa wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika  Jijini Dar es salaam
Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mara baada ya kufungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini na Wadau wa Demikrasia Kutathmini Utekelezaji wa Mpaendekezo ya Kikosi Kazi  na hali ya Siasa Nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam.

No comments