Ni kipi kinamsubiri Yevgeny Prigozhin na mamluki wake huko Belarus baada ya uasi dhidi ya Urusi?
Matukio ya siku za hivi karibuni yanaonyesha jinsi makubaliano kati ya Vladimir Putin na Alexander Lukashenko yalivyokuwa kwamba Yevgeny Prigozhin, atakwenda Belarusi. Hadi sasa, Lukashenka amemwagiza Waziri wa Ulinzi kufuatilia uzoefu wa wapiganaji wa Wagner kwenye mstari wa mbele, licha ya ukweli kwamba Belarus haitapigana na mtu yeyote.
"Marais hao wawili walikubaliana kwamba Rais Lukashenko angeingilia kati kutafuta suluhu ya tatizo hil. Ukweli ni kuwa Alexander Grigoryevich anafahamiana kibinafsi na Prigozhin kwa muda mrefu, takriban miaka 20. Msemaji wa Rais Putin, bwana Dmitry Peskov, alielezea Belarusi iliingilia kati kuzuia jaribio la uasi wa Wagner.
Kwa kweli, urafiki wa karibu kati ya Putin na Prigozhin unatiwa chumvi tu. Kwa mujibu wa machapisho ya MK na AiF, yanasema Prigozhin na Lukashenko walikutana mapema miaka ya 2000 katika mkahawa wa New Island huko St. Petersburg.
Mkahawa ulifunguliwa na Prigozhin, na Putin alipokea wageni kadhaa muhimu huko – mfano Marais Jacques Chirac na George W. Bush. Wakati wa mikutano kama hayo, Prigozhin pia alichukua jukumu la mhudumu. Katika mkahawa huo, Putin pia aliwahi kupata chakula cha jioni na Lukashenko mwaka 2002.
Unaweza kuitwa urafiki usio kamili, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Artem Shraibman aliiambia BBC, na hakuna jambo la maana la kutajwa lililotokea kati yao. Lakini mnamo 2020, wote wawili wakawa mashujaa wa moja ya hadithi za kushangaza za kisiasa za mwaka huo.
Mwishoni mwa Julai 2020, shirika la habari la serikali BelTA, likinukuu vikosi vya usalama, liliripoti njama ilitibuliwa huko Belarus; karibu wanamgambo mia mbili walifika kuchafua hali ya usalama wakati wa kampeni ya uchaguzi.
"Hawakunywa pombe, hawakutembelea vituo vya burudani, walijitenga, wakijaribu kujificha wasingulike," BelTA inaorodhesha miongoni mwa tabia za wageni kutoka Urusi.
Watu 32 kutoka kikundi cha Wagner waliwekwa kizuizini, Lukashenko aliyekasirika aliwaita "majambazi", alizungumza juu ya "nia chafu" kwa upande wa Urusi - na akataka maelezo. Mwanzoni, alikuwa na hakika kwamba watu hawa walitumwa Belarusi ili kuyumbisha usalama katika usiku wa uchaguzi wa rais mnamo Agosti 9, 2020.
Kisha ikawa wazi kuwa majambazi hao hawakuwa na uhusiano wowote na Belarusi, walikuwa ni Wagner PMC na walikuwa wakielekea kwenye moja ya nchi za Kiafrika kupitia Minsk na IIstanbul.
Kisha Lukashenko na Prigozhin waligundua kuwa hawakuwa na lengo la kushambuliana. Prigozhin alimtakia rais wa Belarusi mema. Naye Lukashenko alisema alikuwa na uhusiano mzuri na Wagner.
Mnamo Mei 23, 2021, vikosi vya usalama vya Belarus vililazimisha ndege ya Ryanair iliyokuwa ikiruka kutoka Athens hadi Vilnius kutua Minsk. Wakosoaji wa Lukashenko Roman Protasevich na Sofya Sapega walikamatwa wakiwa ndani ya ndege hiyo. Prigozhin aliunga mkono ukamataji huo.
Mnamo Juni 27, Alexander Lukashenko alithibitisha kwamba Prigozhin alikuwa Belarusi. Ndege yake ya Embraer Legacy 600 (ndege iliyowekewa vikwazo na Marekani), pamoja na ndege ya kusindikiza, kweli zilitua Minsk.
Akaunti kadhaa za Telegra ziliripoti kwamba Prigozhin alionekana kwenye Hoteli ya Green City nje kidogo ya Minsk. Na tarehe 27, ndege zote mbili ziliondoka Minsk na kuelekea Moscow, ikiwa Prigozhin naye alirudi Moscow au la, haijulikani.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alipendekeza kwamba wanachama wa Wagner watie saini mkataba na Wizara ya Ulinzi au waende nyumbani au waende na Prigozhin huko Belarus. Haijulikani kivipi mamluki hao wengi wangevuka mpaka wa Urusi na Belarusi.
Mageuzi makubwa
"Je, wapiganaji wa Wagner watakwenda Belarusi, na lini? Au mpango huo hautafaulu kabisa - bado hatujui lolote kati ya haya, "Artem Shraibman aliambia BBC. Kulingana na yeye, idadi ya mabadiliko ambayo yanaweza kutokea ni makubwa sana kufikia hitimisho.
Taarifa kwa umma kutoka kwa Lukashenko, mtu anaweza kuhitimisha kuwa yeye mwenyewe haelewi nini cha kufanya na watu kutoka kampuni ya kijeshi ya kibinafsi. Kama ilivyo nchini Urusi, uwepo wao haujadhibitiwa kisheria nchini Belarus.
Kwa mfano, katika mkutano na Waziri wa Ulinzi Viktor Khrenin mnamo Juni 27, Lukashenko alisema - mamluki wanaweza kusaidia jeshi la Belarusi na uzoefu wao wa kupigana mstari wa mbele kwa kutumia droni.
"Watakuambia juu ya silaha, ambayo inafanya kazi vizuri, ambayo haikufanya kazi. Na mbinu, na silaha, na jinsi ya kushambulia, jinsi ya kulinda. Hiki ndicho tunachohitaji kuchukua kutoka kwa Wagner,” Lukashenk a alisema.
Aliwahakikishia kuwa wapiganaji wa Wagner hawatalinda silaha za kinyuklia zinazotolewa na Urusi kwa Belarusi. Na hakukataza mamluki hao kujiunga na vikosi vya jeshi la Belarusi.
"Utawala wa Lukashenko una nafasi ya kushiriki katika miradi ya biashara za Prigozhin – zenye utata lakini zenye faida kubwa barani Afrika. Uwezekano wa vikwazo vipya vya Magharibi utaongezeka. Hatari ya Belarusi kuingizwa katika vita na migomo itaongezeka tu," anaandika mwangalizi wa kisiasa Alexander Fridman.
Wakati huo huo, Friedman anabainisha, “mawazo kwamba Wagner watashambulia Kyiv kutoka Belarus ni ya kushangaza." Kwa maoni yake, hii ina maana Minsk itageuka kuwa mshiriki kamili katika vita.
"Siwezi kusema ni kiasi gani watamtishia mtu katika eneo la Belarusi, kwa sababu nadhani kikosi hiki hakitakuwa kikubwa sana," Zelensky alinukuliwa akisema na Ukrayinska Pravda.
Rais wa Poland Andrzej Duda aliita tukio hilo ishara mbaya sana. Naye Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki aliahidi kuwa mpaka wa Belarusi na Poland utaimarishwa zaidi.
Zelensky alielezea kwamba, kulingana na taarifa zake, sehemu kubwa ya Wagner iliharibiwa katika vita, na kwamba jeshi la Ukraine linadhibiti mpaka wa kaskazini.
Kulingana na wachambuzi katika Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita, Belarus haitaweza kuwa kimbilio salama kwa wapiganaji wa Prigozhin ikiwa Kremlin itaanza kuweka shinikizo juu yake.
No comments